Wanafunzi Waimwagia Chuo Kikuu cha Egerton Sifa Chungu Nzima

0
graduates lady KNDI egerton university ongoma

Ni jambo lililotabiriwa kwa namna ambayo ilikwaruza masikio ya wasomi wengi wa chuo cha daraja la kimataifa cha Egerton. Chuo hiki kilionekana kukosa mwelekeo hasa kifedha pale ilipogonga vichwa vya habari kwamba wakurugenzi wakuu huenda wakapiga marufuku ziara za kimasomo kwa ukosefu wa fedha za kutosha. Utabiri ambao wengi waliulaani kwa kuwa ungewasababishia elimu isiyo na manufaa yoyote iwapo ungetimia kama ulivyotabiriwa.

Utabiri huo haukutimia pindi mabasi ya kiakademia yalipoonekana kung’oa nanga yakielekea sehemu mbalimbali nchini Kenya.

Ingawaje kwa sababu za kiusalama ziara nyinginezo ziliwalazimu wasomi kujipata mahala penginepo pasi na walipotarajia huku wengi wao wakishukuru usimamizi wa chuo hicho kwa kuwapa fursa na walichokiita haki yao ya kupata masomo ya kiwango cha juu.Hasa ziara ambazo huwa zinaelekezwa jijini Mombasa zilipata mkondo mpya na wasomi kujipata wakielekea Mashariki mwa Kenya ambapo wangenufaika kwa kuwa usalama Mombasa umebakia kuwa donda sugu ambalo kila kuchapo hutiwa msumari moto.

Wanakitivo cha Elimu na masomo ya jamii walinufaika pakubwa kwa ziara zao hasa walimu-pikwa ambao uhitaji kuufanya utafiti uwandani ili kuwawezesha kuufanya mtihani wao vema.

Isitoshe wanakitivo cha sayansi hasa wale wa baolojia na kemia hawakuficha furaha yao hasa wale waliodai kutobahatika kuwa na ziara yoyote hapa chuoni hadi kufikia mwaka huu wao wa nne.Hilo kwao lilikuwa la kuwapa motisha hasa wanapoukaribia mtihani wao wa mwisho.

Kwa kuzungumza na mmoja wao ambaye alionekana kulifurahia jambo hilo kwa namna isiyofichika,bwana Ando kama alivyojitambulisha alisema kuwa ameyafurahia matunda ya hela zake za karo alizolipia ziara hasa wakati huu anakaribia kutamatisha shahada yake ya kisayansi.

Ingawaje tatizo walilolishuhudia wasomi wengi waliobahatika kujihusisha na ziara hizo ni upungufu wa mabasi huku kikundi kimoja kikilalamikia tukio lililowapata kwa kutembea takriban kilomita tano wakilingoja basi lao lililokuwa limepeleka baadhi ya wasomi wenzao uwandani.

Zaidi ya hayo wasomi hao walionekana kukerwa zaidi kwa kuwa walijazana na kukiuka sheria za barabarani walipotamatisha utafiti wao siku ya Ijumaa ambapo basi lililotengewa idadi isiyozidi wasomi sitini na wawili lililazimika kuwabeba wasomi ziadi ya mia moja ishirini ili kuwasafirisha hadi walipotarajiwa kupumzika.

Lakini wasomi wamebakia kuwapa shukrani wasimamizi wa chuo cha Egerton kwa kuwafikiria na kujizatiti kuwapa mafunzo yenye manufaa kwao.

Comments

comments

Comrade, Share your Thoughts Here

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.